Serikali yatenga trilioni 2.78 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya elimu

0
39

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa amesema Serikali itatumia kiasi cha shilingi trilioni 2.78 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya elimu nchini.

Ameyasema hayo leo Septemba 24, 2022 wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu utekelezaji wa miradi ya elimu, jijini Arusha ambapo amesema Serikali imepanga kuimarisha elimu katika kipindi cha miaka mitano, 2022 hadi 2027 kupitia miradi ya elimu.

Watuhumiwa 15 mbaroni kwa mauaji ya wafugaji Tunduma

Bashungwa amesema kupitia mradi wa kuboresha Elimu ya Sekondari (SEQUIP) utatoa shilingi trilioni 1.2 ili kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu ya Sekondari, kuweka mazingira salama kwa wasichana waliopo katika shule za Sekondari, na kuhakikisha wanafunzi wote wanamaliza elimu hiyo.

Ameongeza kuwa mradi wa kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) utatoa shilingi trilioni 1.6 kwa lengo la kuboresha mazingira ya kusomea, kutoa mafunzo endelevu kwa walimu kazini na kujenga miundombinu ya elimu, huku Programu ya kutekeleza Elimu kwa Matokeo awamu ya Pili (EP4R II) utatoa shilingi bilioni 435.9 kwa lengo la kuendelea kujenga miundombinu mbalimbali ya shule ikiwemo madarasa na nyumba za walimu.

Aidha Waziri Bashungwa amewaagiza Wakuu wa mikoa wote nchini kuhakikisha wanafuatilia miradi yote ya maendeleo ambayo fedha zake zipo kwenye mamlaka za Serikali za Mitaa kukamilika iifikapo Oktoba 1, 2022 na kwamba wakurugenzi watakaoshindwa kukamilisha miradi hiyo taarifa itolewe ili hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao.

Send this to a friend