Serikali yatishia kuwafutia vibali wafanyabiashara wa vyuma chakavu wanaohujumu miundombinu

0
13

Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Mwita Waitara amewataka wafanyabiashara wa chuma chakavu kuwa waaminifu na kuepuka kujihusisha kuhujumu miundombinu.

Waitara ametoa kauli hiyo leo alipofanya kikao na wafanyabiashara hao jijini Mwanza ambapo alionya pamoja na Serikali kuitambua biashara hiyo lakini wapo baadhi ya watu wanaharibu miundombinu na kuwauzia kama chuma chakavu kinyume cha sheria.

Aliwataka wafanyabiashara hao kufanya kazi na Serikali katika kuwafichua wanaoharibu miundombinu kisha kuwauzia kama vyuma chakavu kwani kitendo hicho ni sawa na uhujumu uchumi na wanachafua jina lenu.

“Ukifanya kazi kwa mujibu wa sheria hautagombana na mtu yeyote wa Serikali, umepewa kibali cha kununua chuma chakavu kiwe chakavu kweli na anayekuuzia lazima umfahamu ili tukifuatilia tusikupe mzigo huo na mjua kabisa hili ni jambo baya na kuna wenzenu walikamatwa na wapo katika hatua za kuwajibishwa,” ameonya.

Aidha, ameongeza kuwa ipo haja ya kumshauri Waziri wa Mazingira ambaye ndiye mwenye dhamana ya vibali wapitie upya vibali hivyo na ikibainika wapo wanaohujumu miundombinu kwani wanarudisha nyuma maendeleo ya nchi.

Naibu Wazitri Waitara yupo katika ziara mikoa ya Kanda ya Ziwa kwa lengo la kutoa elimu kuhusu utunzaji wa mazingira akiambatana watendaji kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Send this to a friend