Rais Samia Suluhu Hassan amesema katika hatua za muda mfupi Serikali imetoa shilingi bilioni 10 ili kuimarisha miundombinu ya umeme na kupunguza tatizo la kukatika kwa umeme.
Akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye uwanja wa Police Square wilayani Manyoni mkoani Singida amesema mradi mkubwa wa sola wa dola za Kimarekani milioni 80 unakwenda kujengwa mkoani humo ambao utaongezwa kwenye gridi na kuwezesha upatikanaji wa umeme wa kutosha.
“Katika hatua za muda mfupi, Serikali yenu imetoa bilioni 10 ambazo tunaimarisha miundombinu ya umeme, tunabadilisha nguzo lakini pia tunasimika vikata umeme ili kulinda umeme usikatike katike,” amesema.
Aidha, Rais Samia amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha huduma ya elimu inasogezwa karibu na wananchi ili kuwaondolea watoto adha ya kutembea umbali mrefu, akiongeza kuwa serikali imepiga hatua kubwa katika kupunguza mrundikano wa wanafunzi madarasani kutoka wanafunzi 120 hadi kufikia wanafunzi 45.
Ameongeza kuwa Serikali imejizatiti kuimarisha miundombinu ya barabara na madaraja kote nchini ikiwa ni dhamira yake kutekeleza maendeleo yatakayokwenda kunyanyua wananchi.