Serikali yatoa bilioni 230 za ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi

0
40

Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa imepeleka kiasi cha shilingi bilioni 230 kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya shule za msingi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa mapema Aprili, 2023.

Kupitia fedha hizo kazi zitakazofanyika ni ujenzi wa shule mpya za msingi 302 ambazo zitakuwa na jumla ya madarasa ya awali 604, madarasa ya msingi 3,276, majengo ya utawala 302 pamoja na matundu ya vyoo 6,160.

“Fedha hizi pia zitajenga madarasa kwenye baadhi ya shule za msingi zenye msongamano mkubwa wa wanafunzi unaosababishwa na upungufu wa madarasa ambapo jumla ya madarasa 2,929 yatajengwa katika shule mbalimbali lengo likiwa kupunguza msongamano na kuweka mazingira rafiki ya kujifunza na kufundishia,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, fedha hizo za awamu ya kwanza zitatumika  kukarabati shule za msingi nane zenye uchakavu, madarasa ya awali 368, madarasa ya watoto wenye mahitaji maalumu 41 na mabweni mawili, nyumba za walimu 41 pamoja na matundu ya vyoo 2,899.

Hivyo, ujenzi wa miundombinu hiyo ya elimu ya awali na msingi itakayojengwa kwenye awamu hii ya kwanza itahusisha shule za msingi 1,338.

 

Send this to a friend