
Serikali imetoa jumla ya shilingi Bilioni 5.7 kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Kuboresha Ubora wa Elimu ya Sekondari (SEQUIP) katika Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.
Kati ya fedha hizo, jumla ya shilingi Bilioni 4.450 zimetumika kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mbalimbali katika Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Mkoa wa Kilimanjaro ikiwemo ujenzi wa vyumba vya madarasa, ofisi za walimu, vyoo, maabara, ujenzi wa Bwalo na kadhalika.
Sambamba na fedha hizo pia katika awamu ya pili ya mradi wa SEQUIP serikali imetoa shilingi bilioni 1.1 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa madarasa 10, mabweni 4, nyumba za walimu 3, chumba cha TEHAMA na maktaba.
Wakati huo huo, serikali imetoa kiasi cha shilingi Bilioni 1.6 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule mpya ya Amali ya inayojengwa katika kijiji cha Roseline kata ya Ndumeti katika Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro.
Ujenzi wa mradi huo upo katika hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa, maktaba na jengo la utawala, maabara ya Kemia na Baiolojia pamoja na chumba cha TEHAMA, ujenzi wa choo na mabweni, ujenzi wa karakana ya uashi na umeme, sambamba na bwalo la chakula na nyumba ya mwalimu.








