Serikali yatoa kibali kufungwa ‘cable cars’ Mlima Kilimanjaro
Serikali ya Tanzania imeruhusu ufungwaji wa magari yanayotumia nyanya (cable cars) katika Mlima Kilimanjaro, mlima mrefu zaidi barani Afrika ili kuchochea utalii.
Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari waandamizi jijini Dodoma, Kamishina Msaidizi wa Uhifadhi wa TANAPA, Paul Banga amesema kuwa serikali imeipa TANAPA ruhusa ya kuwekeza katika kufungwa kwa magari hayo.
“Tunasubiria maelekezo kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii kabla hatujaanza kutafuta muwekezaji kwa ajili ya mradi huo,” amesema Banga.
Aidha, amesema kufungwa kwa ‘cable cars’ kwenye milima sio kitu kigeni, huku akiwatoa hofua waongoza watalii kwamba shughuli za kupanda mlima kwa kutembea zitaendelea.
Amesema usafiri huo utawasaidiza zaidi walemavu na watu wenye matatizo ya kiafya ambao hawawezi kitembea umbali mrefu kupanda mlima huo.
Amesema magari hayo yatawekwa hadi umbali wa mita 3,700 kati ya mita 5,895 za mlima huo kutoka usawa wa bahari.
Takribani watalii 50,000 kutoka maeneo mbalimbali duniani hupanda mlima huo kwa mwaka, hata hivyo si wote wanaofaniliwa kufika katika Kilele cha Uhuru.