Serikali yatoa msamaha wa kutoshitakiwa kwa watakaosalimisha silaha haramu

0
120

Jeshi la Polisi limesema Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imetoa msamaha wa kutoshitakiwa kwa wamiliki wa silaha kinyume cha sheria endapo watasalimisha silaha haramu kwa hiari kuanzia leo Septemba 01 hadi Oktoba 31, 2025.

Taarifa hiyo imesema msamaha huo ni moja ya mikakati inayotekelezwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa ikiwemo Tanzania ikiwa ni utekelezaji wa mikataba, itifaki, maazimio na makubaliano mbalimbali ya kuzuia uzagaaji wa silaha ndogo na nyepesi.

Wananchi wametakiwa kuwasilisha silaha hizo katika kituo chochote cha Polisi, ofisi ya Serikali za Mitaa au kwa Mtendaji Kata kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 10 jioni.

“Mtu yeyote atakayepatikana na silaha baada ya kipindi cha msamaha yaani baada ya mwezi Septemba na Oktoba, 2025, atakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria,” imesema taarifa hiyo.

Aidha, wananchi ambao ndugu zao walikuwa wanamiliki silaha kihalali na wamefariki wametakiwa kuhakikisha wanazisalimisha. Pia wamiliki wa silaha ikiwemo kampuni binafsi ambazo zimekua zikiazima au kuazimisha silaha kwa watu wengine zimeonywa kuacha mara moja.

Jeshi hilo imeongeza kuwa silaha zingine zinazotakiwa kusalimishwa ni zile zilizokuwa zinamilikiwa kihalali hapo awali na kampuni binafsi za ulinzi ambazo zimesitisha kutoa huduma za ulinzi na silaha walizokuwa wanamiliki zikarithiwa na kampuni nyingine bila kufuata utaratibu wa kisheria.

Send this to a friend