Serikali yatoa sababu tatu za masoko kuungua moto nchini

0
86

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Jumanne Sagini amebainisha wazi sababu za matukio ya moto kushika kasi kwenye masoko katika maeneo mbambali nchini.

Akizungumza Bungeni Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Cecilia Paresso ambaye alitaka kujua kauli ya Serikali juu matukio hayo ya moto alisema Jeshi la Zima Moto na Uokoaji kwa kushirikiana na vyombo vingine vimebaini kuwa kumekuwa na uunganishwaji holela wa mifumo ya umeme, kutozingatia tahadhari za moto kwa mama lishe na baba lishe pamoja na shughuli za uchomeleaji wa vyuma katika masoko.

Aidha, amesema Serikali kupitia jeshi hilo linashirikiana na halmashauri zote kuboresha miundombinu ya kuzima moto katika masoko na kuhakikisha ramani za masoko mapya zinakaguliwa na vinakidhi vigezo vya kinga na tahadhari.

“Serikali inaendelea kusisitiza uwapo wa vifaa vya awali vya uzimaji moto, uwapo wa ulinzi wa masoko kwa saa 24 na kuzingatia utekelezaji wa mapendekezo ya taarifa maalum za ukaguzi zinazotolewa na Jeshi la Zimamoto na Ukoaji” amesema

Kuhusu suala la kulipwa fidia kwa wahanga wa moto amesema hilo ni jambo la kisheria na Bunge halijapitisha utaratibu wa namna hiyo huku akisisitiza kuwa muhimu ni elimu ya kinga dhidi ya majanga haya ili yasitokee.