Serikali yatoa tahadhari ugonjwa wa Ebola

0
31

Wizara ya Afya imewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ebola ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maji safi na sabuni, kuepuka kugusa mwili au majimaji ya mwili wa mhisiwa au mgonjwa wa Ebola, na kuepuka safari zisizo za lazima.

Kupitia taarifa iliyotolewa kwa umma, Wizara imesema Septemba 20, 2022 ilipata taarifa kupitia vyombo vya habari juu ya mlipuko wa ugonjwa wa huo nchini Uganda, ikieleza mgonjwa aliyethibitika kuwa na Ebola amefariki wilayani Mubende nchini humo.

Aidha, wizara imesema hadi sasa hakuna mgonjwa wa Ebola nchini, na kwamba imewaagiza waganga wakuu wa Mikoa na Halmashauri kuimarisha utoaji wa elimu, ufuatiliaji wa ugonjwa, uchunguzi wa kitaalam, kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba na kinga muhimu katika maeneo yao, na vile vile uchunguzi wa wageni wanaoingia nchini kupitia mipaka.

Dalili kuu za ugonjwa huo ni pamoja na homa kali inayoambatana na kutokwa damu katika matundu ya mwili yaani pua, njia ya haja kubwa na ndogo, mdomoni, masikioni na machoni, hali inayopelekea kifo kwa muda mfupi. Ugonjwa huo unaenea kwa kugusa majimaji ya mwili wa mgonjwa mfano mate, damu, mkojo na machozi.

Send this to a friend