Serikali yatumia bilioni 2.4 kugharamia timu za Taifa

0
47

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro amesema katika kipindi cha Julai 2023 hadi Februari, 2024 wizara kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) imetumia shilingi bilioni 2.4 kugharamia timu mbalimbali za Taifa katika mashindano ndani na nje ya nchi.

Amesema hayo wakati akiwasilisha utekekezaji wa Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2023/2024 na Mpango wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwenye Kamati ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo Bungeni Jijini Dodoma.

Amezitaja baadhi ya timu hizo kuwa ni Timu ya Taifa ya Gofu Wanawake iliyoshiriki mashindano ya Gofu Afrika Mashariki na Kati nchini Rwanda, Timu ya Wanawake ya Mpira wa Miguu (Twiga Stars) ambayo iliwezeshwa kushiriki michuano ya kufuzu kucheza WAFCON Juni, 2024, kuwezesha Timu nane ikiwemo Judo, Riadha, Mpira wa Miguu Wanawake, ngumi, kriketi wanaume, na Wanawake kushindana mashindano ya Michezo Afrika (All African Games) yanayoendelea nchini Ghana.

Aidha, amesema kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Februari 2024, wizara imetumia takriban bilioni 10.17 kwa ajili ya miradi ya maendeleo ikiwemo mradi wa ujenzi wa eneo changamani la michezo, ukarabati wa Uwanja wa Benjamin Mkapa, ujenzi wa vituo vya mazoezi na kupumzikia Dodoma na Dar es Salaam, na ujenzi wa hosteli za Chuo Cha Michezo Malya ambao unaendelea.

Send this to a friend