Serikali yawaonya madereva wanaohamasisha mgomo

0
40

Serikali imewaonya baadhi ya madereva wanaopotosha taarifa iliyotolewa na Serikali Julai 22, mwaka huu kuhusu hatua zilizochukuliwa katika kushughulikia hoja na malalamiko yaliyowasilishwa na viongozi wa vyama vya wafanyakazi madereva na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji nchini.

Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako amesema, kufuatia taarifa hiyo wapo baadhi ya madereva ambao wamekuwa wakipotosha taarifa hiyo na kuchochea ama kuhamasisha madereva wenzao kugoma.

“Uchochezi wa mgomo wao umejikita katika viwango vya posho ambavyo madereva, wamiliki wa vyombo vya usafiri na Serikali waliafikiana katika vikao vya majadiliano” amesema.

Amesema viwango walivyokubaliana ni viwango vya chini vya posho za safari (Minimum allowances) ambapo waajiri hawaruhusiwi kulipa chini ya viwango hivyo na kwa wale waajiri waliokuwa wanalipa viwango ambavyo viko juu ya viwango vya chini vya posho za safari vilivyowekwa, hawaruhusiwi kushusha viwango hivyo kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Aidha, Serikali imesisitiza kuwa nafasi ya majadiliano bado ipo wazi na hivyo wafanyakazi madereva wenye hoja na malalamiko zaidi ya yale yaliyofanyiwa kazi, wayawasilishe rasmi katika mamlaka zinazohusika ili yapatiwe ufumbuzi.

“Natoa rai kwa makundi yanayojihusisha kuchochea migomo ya madereva kuacha mara moja, kwani kufanya hivo ni kukiuka sheria. Hivyo Serikali haitasita kuchukua hatua stahiki kwa wale wote watakaoendelea kuchochea migomo ya madereva,” amesisitiza.

Send this to a friend