Kampuni ya Ranchi za Taifa Limited (NARCO) imetoa wito kwa viongozi wa mikoa nchini kujenga utaratibu wa kufanya matamasha ya ulaji nyama ili kuhamasisha wananchi kuongeza wigo wa kula nyama, kujenga afya zao na kuongeza uzalishaji wa bidhaa hiyo nchini.
Meneja Masoko wa NARCO Bw. Immanuel Mnzava amesema uhamasishaji unahitajika ili kuongeza ulaji wa nyama nchini kwa kuwa kwa mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO), ulaji wa nyama nchini kwa mtu mmoja bado uko chini ambapo ni wastani wa Kilogramu 15 kwa mwaka tofauti na pendekezo la dunia la ulaji wa Kilogramu 50 kwa mwaka.
“Ulaji unaopendekezwa duniani ni Kilogramu 50 kwa mwaka. Kwa hiyo kwa wastani kila mwananchi ili afikie viwango vya ulaji nyama vinavyopendekezwa duniani anadaiwa kuongeza Kilogramu 35 ili afikishe kilo 50 kwa mwaka, ili kufikia viwango hivyo, Tanzania inadaiwa wastani wa tani za nyama 2,100,000 kwa mwaka,” amesema Mnzava.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joseph Mkirikiti akizungumza juu ya tamasha la Sumbawanga Nyama Choma Festival amesema ni moja ya vyanzo vya mapato na matamasha hayo yatafungua fursa ya utalii wa ndani nchini.