Serikali yaweka ukomo wa bei kwa bidhaa inazonunua

0
46

Serikali imeeleza kuwa imeweka ukomo wa bei za bidhaa ambazo Serikali inanunua kwa kuzingatia bei za soko ili kudhibiti ununuzi wa bidhaa hizo kwa gharama kubwa kuliko zilizopo Sokoni.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum, Asia Halamga, aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu kushusha gharama za ununuzi na kuagiza bidhaa hususani magari kulingana na bei ya Soko.

“Ukomo wa bei za manunuzi ambayo Serikali inafanya si tu kwa magari lakini pia kwa bidhaa nyingine, kuanzia mfumo wenyewe wa manunuzi ambapo Afisa Masuuli anapotaka kulipa kwa gharama za juu kuliko bei ya soko inayotambulika atakuwa amekiuka Sheria,” amesema Dkt. Nchemba.

EWURA yabadili utaratibu kwa waagizaji mafuta

Amesema mtazamo wa Serikali ni kuendelea kupunguza matumizi ya magari ambapo Serikali iliweka utaratibu kwa wale wenye sifa ya kuwa na magari wakopeshwe ili kuipunguzia Serikali mzigo wa kuyaendesha na kuyafanyia huduma za matengenezo.

Kuhusu Wakala wa Huduma ya Ununuzi Serikalini (GPSA) kuchelewesha ununuzi wa magari ya Serikali, Dkt. Nchemba amesema ucheleweshaji huo ulisababishwa na Mabadiliko ya aina (models) za magari yanayotumiwa na Serikali ambapo upatikanaji wa aina mpya huweza kuchukua muda mrefu zaidi kutegemea na idadi ya mahitaji kwa Serikali.

Send this to a friend