Serikali yaziunganisha benki zake za biashara na kuunda benki moja

0
36

Serikali ya Tanzania imeziunganisha benki zake mbili za biashara, Benki ya Posta Tanzania (TPB) na Benki ya TIB Corporate kuanzia leo Juni 01, 2020.

Msajili wa Hazina, Athumani Mbuttuka amesema kuwa uamuzi huo unalenga kuwa na benki moja ambayo itakuwa imara pia utaleta mageuzi makubwa ya kiutendaji, kimfumo, kimuundo na kitaswira ili iweze kuhimili ushindani wa kibiashara kwenye sekta ya fedha.

“Uamuzi huu ni adhma ya serikali ya kuwa na benki moja ya biashara ya serikali ambayo ni imara na yenye ufanisi, hivyo nampongeza Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa maoni, dhamira na uongozi thabiti unaolenga kuboresha utendaji wa mashirika na taasisi za umma,” amesema msajili.

Akitoa ufafanuzi zaidi Mbuttuka amesema kuwa muungano huo unaifanya benki mpya kuwa na mali zenye thamani ya takribani TZS 1 trilioni, na kwa hatua ya awali, Benki ya TPB itachukua mali na madeni ya Benki ya TIB Corporate.

Katika kuwatoa hofu wananchi Mbuttuka ameuhakikishia umma kuwa serikali itaendelea kuhakikisha utendaji wa benki zake unaimarika na maslahi ya wenye amana na wateja wote yanalindwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za usimamizi wa benki na taasisi za fedha.

Amesema wateja wataendelea kupata huduma kwenye matawi yao ya sasa hadi hapo watakapotaarifiwa vinginevyo na kuwa huduma za kibenki hazitaathirika kwa vyovyote vile kutokana na mabadiliko haya.

Send this to a friend