Seven Mosha ateuliwa kusimamia Sony Music ukanda wa Afrika Mashariki

0
47

Sony Music Entertainment Africa imemteua Christine Mosha, maarufu Seven, kusimamia Masoko na Maendeleo ya Wasanii katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Seven ambaye amefanya kazi na wasanii wengi wa Afrika Mashariki ana uzoefu wa zaidi ya miaka 15 katika masuala ya burudani. Mwaka 2017 alianzisha lebo yake ya Rockstar Africa na kuwasimamia wasanii mbalimbali akiwa ni pamoja na Lady Jaydee, Ray C, TID, Rose Muhando, Xtatic, Alikiba na Ommy Dimpoz.

“Kwa miaka mingi tayari amekuwa mshirika wetu, akitupatia ushauri namna ya kufanya kazi Afrika Mashariki, eneo ambalo ni muhimu na lenye nguvu ya muziki Afrika. Hivyo tunafuraha kuwa naye, kwani atasaidia kuongeza orodha yetu ya wasanii Afrika Mashariki na kuonesha hazina yetu ya kimataifa kwa mashabiki wapya,” amesema Sean Watson, Mkurugenzi Mtendaji wa Sony Music Africa.

Kwa upande wake Seven amesema “Sony Music ina historia kubwa katika sekta ya burudani duniani, hivyo kuwa sehemu ya kampuni hii kwa wakati huu katika kazi yangu naona ni hatua kubwa sana kwani nitaweza kuleta uzoefu wangu kwenye taasisi hii kwa ujumla.”

Ameongeza kuwa anaamini kujiunga kwake na Sony Africa kutakiwa na matokeo chanya katika maendeleo ya muziki si tu Afrika Mashariki bali Afrika kwa ujumla.

Tangu 2010 amekuwa akifanya kazi na Rockstar 4000 Music Entertainment ambapo akiwa hapo aliweza kufanya masuala mbalimbali ya muziki kwa kushirikiana na Sony Music Africa ikiwa ni pamoja na kushirikiana katika kampeni ya Kombe la Dunia mwaka 2010 lililofanyika Afrika Kusini.

Kuanzia 2005 hadi 2010 amefanya kazi na MTV Networks Africa akishughulia masuala ya ubunifu (brand) na biashara.

Send this to a friend