SGR Dar-Moro kuanza kutumika Agosti 2021

0
15

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa amesema kuwa majaribo ya treni ya abiria yanatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi Agosti, 2021 kwa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro.

Kadogosa amesema hilo Ikulu, Dar es Salaam leo alipokutana na kufanya mazumzo na Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu maendeleo ya miradi ya ujenzi wa reli na maendeleo ya TRC.

Amemshukuru Rais Samia kwa kuidhinisha kiasi cha shilingi bilioni 372.34 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa kipande cha 5 cha reli ya Mwanza – Isaka chenye urefu wa kilometa 341 kwa kiwango cha kisasa (standard gauge railways).

Aidha, ameeleza kuwa tangu Rais Samia aingie madarakani ujenzi wa reli katika vipande 2 unaendelea vizuri ambapo hadi mwezi uliopita kipande cha Dar es Salaam – Morogoro (kilometa 300) kilikuwa kimefikia ya asilimia 91 na Morogoro – Makutupora (kilometa 422) kilikuwa kimefikia asilimia 60.02.

Kwa upande wake, Rais Samia amesema Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuhakikisha ujenzi wa reli ya kati utakaounganisha Bandari ya Dar es Salaam na Mikoa ya Kanda ya Ziwa na Kanda ya Magharibi unakamilishwa ili kuzifikia nchi za Uganda, Burundi, Rwanda na DRC.

Amemtaka Kadogosa kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo ya ujenzi vizuri ikiwa ni pamoja na kujipanga kwa ajili ya ujenzi wa vipande vya Makutopora – Tabora, Tabora – Isaka na Kaliua – Mpanda – Kalema.

Send this to a friend