Shabiby aipa serikali mbinu rahisi ya kupunguza bei ya mafuta

0
43

Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby ameiomba Serikali kubadili utaratibu unaotumika kwa sasa katika uagizaji wa mafuta nchini ili kuepuka changamoto zinazojitokeza mara kwa mara ya kupanda kwa bei ya mafuta.

Akizungumza bungeni jijini Dodoma wakati akichangia mjadala wa makadirio ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka 2022/23, mbunge huyo amesema utaratibu unaotumika kwa sasa wa kuaguza mafuta kwa pamoja (bulk procurement) hauleti ushindani, hivyo kusababisha mafuta kuuzwa kwa bei moja hata kama mfanyabiashara anataka kuuza kwa bei ya chini.

“Kuwepo kwa vita ya Urusi na Ukraine kwa Tanzania ni fursa, na kwa nchi zingine ni fursa ya kupata mafuta kwa bei rahisi lakini kwetu sisi imekuwa ni moto,” amesema Shabiby.

Pia ameeleza kuwa, Serikali ikiruhusu wafanyabiashara binafsi kuleta mafuta nchini ni rahisi na bei itakuwa chini kuliko walivyotegemea, huku EWURA, TBS kazi yao ibaki kupanga bei na kiwango kinachohitajika.

“Serikali kazi yake iwe kuangalia tu kiwango wanachokitaka na bei inayotakiwa. Vitu vingine wanatunga tu kwamba ukileta mafuta mtu mmoja mmoja yatakuwa yanakwepa ushuru, meli zote zinashushwa kwenye mita, zinashushia wapi? Hii kazi iachieni TRA, wanafanya kazi nzuri waaminini,” ameongeza.

Ametolea mfano kipindi cha nyuma ambao kampuni moja kutoka India ilikuwa ikiingiza mafuta nchini na bei ikawa nafuu, lakini ilipigwa mizengwe na kuamua kuiuza kampuni hiyo, wawekezaji wakaondoka.

Send this to a friend