Sheikh wa Mkoa ahukumiwa kifungo kwa kummwagia mwanamke maji ya moto

0
45

Mahakama ya Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi imemhukumu kwenda jela miezi sita au fani TZS 50,000 Sheikh wa Mkoa wa Katavi, Mashaka Nassoro maarufu kama ‘Kakukulu’ kwa kosa la kumshambulia Asha Aman kwa kummwagia maji ya moto na kumsababishia majeraha makubwa Februari 28, mwaka jana.

Mshtakiwa huyo alipandishwa kizimbani na kusomewa shtaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama, Gosper Luoga akituhumiwa kutenda kosa hilo kinyume na kifungu cha 225 cha kanuni ya adhabu, cap 16 R.E 2021.

Hakimu alisema kuwa, kwa upande wa mashtaka umejiridhisha na kuthibitisha kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo na Mahakama inamtia hatiani

Inaelezwa kuwa siku hiyo Bi. Asha alikwaruzana na Mwajuma Haruna ambaye ni shemeji wa Sheikh Nasoro, ndipo walianza kushambuliana kwa matusi ambayo mshatakiwa aliyasikia baada ya kufika nyumbani hapo na kuanza kumtukana mlalamikaji.

Baada ya hapo ilielezwa kuwa mshtakiwa alimshika shingo na kuanza kumpiga mlalamikaji kisha kuchukua maji ya moto na kumwagia mwilini

Mlalamikaji aliliripoti tukio katika kituo cha polisi na kupewa PF3 kwa ajili ya kupatiwa matibabu katika hospitali ya Mkoa wa Katavi na kulazwa hospitalini hapo kwa wiki moja.

Hata hivyo mtuhumiwa alikwepa kifungo cha kwenda jela kwa kulipa faini ya TZS 50,000

Send this to a friend