Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana amesema jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika katika kuhakikisha katiba mpya inapatikana lakini Rais Samia Suluhu Hassan ameonesha dhamira na kutekeleza kwa vitendo ili kuhakikisha jambo hilo linafanikiwa.
Akizungumza leo katika mkutano wa kitaifa wa wadau kujadili hali ya demokrasia nchini kuelekea uchaguzi mkuu wa Serikali za mitaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ulioandaliwa na Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), amesema Serikali inafanya mchakato wa aina mbili kuhakikisha katiba mpya inapatikana.
“Mchakato wa kwanza ni wa kutafuta namna ya kupata katiba, lakini kwa sababu mchakato huu utachukua muda kuna mchakato wa pili ambao ni wa kurekebisha maeneo matatu ambayo yanahusu uchaguzi, huu ni kwa ajili ya uchaguzi wa 2024 na 2025.
Rais Samia: Hakuna mwenye ubavu wa kuligawa au kuliuza Taifa hili
Ya kwanza ni sheria inayohusu tume ya uchaguzi, ya pili ni sheria inayohusu uchaguzi wenyewe utakavyoendeshwa na ya tatu ni sheria inayohusu namna vyama vya siasa vitakavyosimamiwa,” amesema.
Kinana ameongeza kuwa “mimi nina hakika sheria hizi tatu zikitazamwa na sote kwa pamoja tukikubaliana kupitia vikao kama hivi kupitia TCD na baraza la vyama nina hakika tutakuwa na uchaguzi ulio huru na wa haki zaidi kuliko wakati wowote mwingine kutoa nafasi kwa Watanzania kuwachagua wale ambao wangependa wawe wawakilishi katika vyombo vya uwakilishi.