
Uchambuzi mpya wa kiuchumi umeonesha kuwa shilingi ya Tanzania imeendelea kuwa imara licha ya kuongezeka kwa deni la taifa, hali inayotajwa kuchangiwa na uwepo wa akiba ya fedha za kigeni, mikakati madhubuti ya sera za fedha unaofanywa na Benki Kuu ya Tanzania pamoja na udhibiti wa mikopo ya ndani.
Kwa mujibu wa uchambuzi huo uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Kiuchumi ya TICGL wa mwezi Desemba 2025, thamani ya Shilingi ya Tanzania imeonesha utulivu mkubwa dhidi ya Dola ya Marekani, ambapo wastani wa ubadilishaji ulifikia Shilingi 2,452.76 kwa dola moja, huku kiwango cha kushuka kwa thamani ya fedha hiyo kwa mwaka kikiwa asilimia 1.3 pekee, kiwango kinachotajwa kuwa kidogo ukilinganisha na nchi nyingine za ukanda huo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa deni la taifa limefikia shilingi trilioni 134.9, ambapo sehemu kubwa ya deni hilo ni la nje linalochukua takribani asilimia 69.5 ya jumla ya madeni yote, huku deni la ndani likichangia asilimia 30.5.
Hata hivyo, wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa licha ya ukubwa wa deni la nje, hali bado inadhibitika kutokana na uwepo wa akiba ya fedha za kigeni inayokadiriwa kufikia shilingi trilioni 15.5 pamoja na mapato ya mauzo ya nje yanayotokana na dhahabu, utalii na kilimo.
Aidha, muundo wa deni la ndani umetajwa kusaidia kulinda uthabiti wa shilingi, kwani sehemu kubwa ya deni hilo ipo katika mfumo wa hati fungani za muda mrefu zinazopunguza presha ya ulipaji wa haraka wa madeni. Vilevile, wadai wakuu wa deni la ndani ni taasisi za ndani kama benki za biashara, mifuko ya hifadhi ya jamii na Benki Kuu ya Tanzania.
Ripoti hiyo pia inaeleza kuwa malipo ya deni la ndani hufanyika kwa kutumia shilingi ya Tanzania, jambo linalosaidia kupunguza utegemezi wa fedha za kigeni na kulinda thamani ya sarafu hiyo.
Pamoja na mafanikio hayo, wataalamu wameonya kuwa ni muhimu kuendelea kudhibiti ukopaji, kuimarisha mauzo ya nje na kufuatilia mwenendo wa uchumi wa dunia ili kuhakikisha uthabiti wa shilingi unaendelea kudumu.






