Shilingi ya Tanzania yaimarika na kuwa miongoni mwa sarafu zinazofanya vizuri zaidi duniani

0
3

Shilingi ya Tanzania imeimarika kwa kasi na kuwa miongoni mwa fedha zinazofanya vizuri zaidi duniani kutokana na kuongezeka kwa mapato ya Dola kutoka sekta za dhahabu, kilimo, utalii na usafirishaji, pamoja na kanuni mpya zilizowekwa kuhusu matumizi ya fedha za kigeni nchini.

Mkurugenzi wa Masoko ya Fedha wa kutoka Benki ya Tanzania (BoT), Emmanuel Akaro, amesema sababu kubwa ya kuimarika kwa shilingi ni kupanda kwa bei ya dhahabu duniani, ambapo sasa inauzwa zaidi ya Dola 3,300 kwa wakia moja. Tanzania huzalisha wakia milioni 1.9 za dhahabu kwa mwaka, hivyo mapato kutoka sekta hiyo yameongezeka kwa karibu Dola bilioni 2.

Kwa mujibu wa BoT, leo shilingi inauzwa kati ya TZS 2,578 na TZS 2,604 kwa Dola moja ya Marekani, ikilinganishwa na TZS 2,586 hadi TZS 2,612 mwanzoni mwa Machi.

Akaro ameongeza kuwa sekta ya utalii nayo imechangia kwa kiasi kikubwa, ambapo mwaka jana Tanzania ilipokea watalii milioni 2.6 walioliingizia Taifa Dola bilioni 3.9 ikiwa ni ongezeko kubwa ikilinganishwa na Dola milioni 715 zilizopatikana mwaka 2020 wakati wa janga la UVIKO-19.

Kwa upande wa kilimo, mauzo ya zao la ufuta kupitia soko la TMX yamekuwa yakileta mamilioni ya Dola kila siku, huku kilo moja ya ufuta ikiuzwa hadi zaidi ya TZS 3,000. Pia, mauzo ya tumbaku msimu huu yanatarajiwa kuingiza Dola milioni 400.

Akaro amesema kwa kuwa misimu ya kilimo na utalii inaendelea, na kwa kuzingatia hali nzuri ya uchumi kama ukuaji wa Pato la Taifa kwa 6%, mfumuko wa bei wa 3%, na akiba ya fedha za kigeni ya dola bilioni 5.5, shilingi inatarajiwa kuendelea kuimarika hadi mwisho wa mwaka huu.

Kwa upande wa usafirishaji, Akaro amesema sekta ya usafirishaji imeonesha mafanikio ambapo meli na malori ya mizigo kutoka nchi jirani yanayopitia Tanzania hulipa huduma kwa Dola, na hivyo kuongeza mapato ya kigeni.

Akaro anasema hali ya sasa ni ya kihistoria kwa sababu hata benki za biashara zina ziada ya Dola na zinaiomba BoT kununua Dola kutoka kwao. Hii ni kutokana na kupungua kwa mahitaji ya Dola baada ya kukamilika kwa miradi mikubwa kama Bwawa la Nyerere na kushuka kwa bei ya mafuta duniani kutoka Dola 100 hadi Dola 65 kwa pipa.