Shirika la Afya Duniani (WHO) limebadilisha ushauri wake kuhusu uvaaji wa barakoa, ambapo sasa limesisitiza uvaaji (wa barakoa) katika maeneo yenye watu wengi ili kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona.
Shirika hilo lenye dhamana ya kusimamia afya za watu limesema kuwa taarifa mpya inaonesha kuwa barakoa zinaweza kuzuia matone ya mate au makamasi yenye maambukizi kwenda kwa mtu mwingine.
Ushauri huo unakuja wakati tayari baadhi ya nchi zimeweka sharti kwa wananchi kuvaa barakoa wakati wote wanapokuwa katika maeneo yenye watu wengi.
Awali shirika hilo lilisema kwamba hakukuwa na ushahidi wa kutosha wa kuwafanya watu wasio na maambukizi kuvaa barakoa.
Dkt. Maria Van Kerkhove amesema kuwa pendekezo hilo jipya linahimiza uvaaji wa barakoa za vitambaa (zisizo za kitabibu) kwenye maeneo yenye hatari ya kusambaa kwa ugonjwa wa homa ya mapafu (Covid-19).
WHO imekuwa ikisisitiza kuwa barakoa za kitabibu zivaliwe tu na wenye maambukizi ya virusi hivyo pamoja na matabibu wanaowahudumia wagonjwa.
Hata hivyo WHO imesisitiza kuwa uvaaji wa barakoa ni moja ya nja za kujikinga na maambukizi ya Covid-19, na si njia pekee, kwamba mtu akivaa barakoa bila kuchukua tahadhari nyingine anajiweka katika hatari ya kupata maambukizi.