Shitaka linalomkabili mume anayedaiwa kumtoboa macho na kumng’oa jino mkewe

0
43

Mwanaume anayedaiwa kumshambulia mke wake, kumtoboa macho na kumng’oa jino, Isack Robertson (45) amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Arusha.

Mtuhumiwa huyo mkazi wa Sombetini jijini Arusha amefikishwa mahakamani hapo leo na kusomewa shitaka moja la shambulio la kudhuru mwili.

Imeelezwa mahakamani hapo kuwa Mei 23, 2023 mtuhumiwa alipofika nyumbani alielekea chumbani moja kwa moja bila salamu, na mkewe, Jackline Mkonyi (38) aliamua kumfuata na ndipo alipomvuta hadi sebuleni na kuanza kumpiga mateke, kumpiga kwa mkanda wake wa suruali maeneo mbalimbali ya mwili wake na kumng’oa jino kwa kutumia plaizi jambo lililomfanya mwathirika atokwe na damu nyingi.

Mwanaume aomba mahakama ivunje ndoa yake kutokana na uzuri wa mkewe

Imeelezwa kuwa baada ya shambulio hilo, mtuhumiwa alimpigia mama mkwe wake na kumweleza kuwa ajiandae kupokea mzoga wake, kisha alimpeleka mkewe nyumbani kwao na kumtelekeza nje ya geti na yeye kutokomoea kusikojulikana hadi alipokamatwa Mei 27 eneo la Himo, Kilimanjaro.

Baada ya kusomewa kosa hilo, mtuhumiwa huyo alikana kutenda kosa hilo ambapo upande wa jamhuri ulieleza kuwa upelelezi umekamilika na kumsomea maelezo ya awali ambapo pia wamewasilisha maombi madogo ya kuomba mshitakiwa huyo asipewe dhamana kwa sababu ya usalama wake na usalama wa mwathirika.

Kufuatia maombi hayo hakimu aliahirisha kesi hiyo kwa muda kwa ajili ya kutolea uamuzi mdogo.

Send this to a friend