Shule Kenya zaamriwa kurejesha ada za wanafunzi

0
43

Waiziri wa Elimu nchini Kenya ameziagiza shule nchini humo kurejesha ada za wanafunzi kwa mwaka 2020 au wazipeleke mbele zitumike shule zitakapofunguliwa mwaka 2021.

Waziri George Magoha amesema hayo wakati akijibu moja ya hoja iliyoibuka muda mfupi baada serikali kutangaza kuwa shule zote za msingi na za sekondari zitafunguliwa mwaka 2021.

Akitolea ufafanuzi suala hilo Magoha amesema kuwa visa vya corona vinaongezeka nchini humo, na hivyo shule zitakapofunguliwa mwakani wanafunzi wataendelea kwenye ngazi waliyopo sasa.

Ameongeza kuwa hata wanafunzi waliokuwa katika miaka yao ya mwisho wa masomo au waliopaswa kufanya mitihani ya taifa hawatofanya.

Wazazi nchini humo wamekuwa na mitazamo tofauti ambapo baadhi wanahoji uhalali wa shule kuwataka kulipia madarasa kupitia mitandao wakati watoto wao watatakiwa kurudia darasa. Lakini kwa upande mwingine baadhi yao wamesema madarasa hayo ni njia bora ya kuhakikisha watoto wanaendelea kujifunza.