Shura ya Maimam: Wamemkamata Sheikh Ponda ila maandamano yako pale pale

0
51

Baada ya Jeshi la Polisi kuthibitisha kumkamata Katibu Mkuu wa Shura ya Maimam, Sheikh Ponda Issa kwa madai ya kutaka kuongoza maandamano yaliyopangwa kufanyika Novemba 10, mwaka huu Dar es Salaam, taasisi hiyo imesema kilichofanywa na polisi ni ukiukwaji wa sheria.

Akizungumza na wanahabari Jumamosi Novemba 11, 2023 Amiri wa Habari wa Shura ya Maimam, Abubakari Mngodo amesema taasisi hiyo itaendelea kupaza sauti kwa kuwa nia ya maandamano iko palepale, na kwamba taasisi ilitoa taarifa ya maandamano hayo tangu Novemba 3, mwaka huu.

“Tulitoa taarifa kuanzia Novemba 3, 2023 lakini leo tunazuiwa na hatukupewa taarifa yoyote, kama walikuwa hawajaridhia wangetujibu kwa barua kama sisi tulivyopeleka barua,” amesema Mngodo.

Ameongeza kuwa kwenye maandamano hayo watu waliokamatwa ni 11 na walioachiwa ni wanawake watatu, huku watu nane wakiendelea kushikiliwa akiwemo Shekh Ponda.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Sheikh Ponda alikamatwa Novemba 10, 2023 katika viwanja vya Mnazimmoja wakati akizungumza na waandishi wa habari kabla ya kuongoza maandamano hayo yaliyolenga kupinga kile kinachodaiwa kuwa uvunjfu wa haki za binadamu kwa Wapalestina.