Siku ya Figo Duniani: Mambo rahisi ya kufanya kuepuka ugonjwa wa Figo

0
15

Kila Alhamisi ya wiki ya pili ya mwezi Machi, dunia huadhimisha Siku ya Figo Duniani. Siku hii ilianza kuadhimishwa rasmi mwaka 2006 katika nchi 66 na baadaye kuenea katika nchi zote duniani. Nchini Tanzania ilianza kuadhimishwa mwaka 2011.

Ikiwa leo Machi 09, 2023 ni maadhimisho ya ugonjwa huo, Wizara ya Afya imesema ugonjwa wa figo unaathiri asilimia 7 ya Watanzania huku idadi ya wagonjwa imekuwa ikiongezeka kwa kiasi kikubwa jambo linaloashiria ukubwa wa tatizo hili nchini.

Magonjwa ya figo hutokana na sababu mbalimbali kulingana na umri wa mwathirika ikiwemo shinikizo la damu, kisukari, magonjwa yanayotokana na matatizo ya mfumo wa mkojo, matumizi ya mitishamba na matumizi holela ya dawa mbalimbali zinazoathiri figo ikiwa ni pamoja na dawa za maumivu kama diclofenac.

Yafuatayo ni mambo ya kuzingatia kila siku ili kujiepusha na ugonjwa wa figo;

1. Fanya mazoezi
Mazoezi ya kila mara na shughuli za kimwili za kila siku hudumisha msukumo wa kawaida wa damu na hudhibiti kisukari. Shughuli za kimwili huondoa hatari ya kisukari, na msukumo wa juu wa damu hivyo kupunguza hatari ya ugonjwa sugu wa figo.

2. Lishe bora
Kula lishe yenye afya, matunda na mbogamboga. Punguza ulaji wa vyakula vilivyosagwa, sukari, mafuta, nyama na chumvi hasa baada ya umri wa miaka 40 kwani itasaidia kuzuia msukumo wa juu wa damu na kuwepo kwa mawe ya figo.

3. Zingatia uzito wako
Hakikisha una uzito sawa kwa kula lishe bora na mazoezi stahiki. Hii inaweza kuzuia kisukari, magonjwa ya moyo, magonjwa sugu ya figo na hali nyingine zinazohusishwa na ugonjwa sugu wa figo.

Daktari: Mtu anatakiwa kufanya ngono mara tatu kwa wiki

4. Acha uvutaji wa tumbaku
Uvutaji wa tumbaku na matumizi mengine ya tumbaku yanaweza kusababisha ‘atherosclerosis’. Hii inaweza kupunguza mtiririko wa damu hadi kwenye figo na hivyo kupunguza uwezo wa figo kufanya kazi vyema.

5. Jihadhari na OTCs
Jihadhari na matumizi ya dawa za kupunguza/kutuliza maumivu zinazonunuliwa bila maagizo ya daktari. Dawa kawaida kama non-steroidal anti-inflammatory, ibuprofen zinajulikana kusababisha uharibifu wa figo na hitilafu ya figo zikitumika mara kwa mara. Pata ushauri wa daktari jinsi ya kudhibiti maumivu yako bila kuhatarisha figo zako.

6. Kunywa maji mengi
Unywaji wa maji ya kutosha (kiasi cha lita 3 kila siku) husaidia kuzimua mkojo, kutoa uchafu wote wa sumu kutoka mwilini na kuzuia mawe kwenye figo.

7. Uchunguzi wa figo wa kila mwaka
Magonjwa ya figo huwa magonjwa yanayoingia mwilini kimya kimya na hayatoi dalili zozote hadi yafikie hatua ya kuimarika. Mbinu sahihi na bora ni uchunguzi wa mara kwa mara.