Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP), Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) na Shirika la Aids Healthcare Foundation (AHF) kwa pamoja wataadhimisha siku ya Kondomu Duniani kwa mara ya kwanza nchini Februari 13, 2025.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa Habari, Kaimu Meneja Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI Magonjwa ya Ngono na Homa ya Ini (NASHCoP), Dkt. Zeye Nkomela amesema maadhimisho hayo yatafanyika mkoani Dodoma.
Dkt. Nkomela amesema katika kutekeleza azma ya Serikali ya kutokomeza janga la UKIMWI ifikapo mwaka 2030 kwa mwaka 2025, Wizara imeamua kujumuika na mataifa mengine Duniani ambayo yamekuwa yakiadhimisha siku ya Kondomu tangu mwaka 2009, kama sehemu ya dhamira ya kupambana na kuenea kwa maambukizi ya VVU na magonjwa ya ngono.
“Katika maadhimisho hayo shughuli mbalimbali zitafanyika ikiwemo kuwakumbusha watu juu ya umuhimu wa kujikinga na VVU na UKIMWI, magonjwa ya ngono na mimba zisizotarajiwa, utoaji wa elimu juu ya matumizi sahihi ya kondomu na kuhamasisha upatikanaji wa kondomu kwa wananchi,” amesema Dkt. Nkomela.
Pia Dkt. Nkomela amesema Serikali imeamua kuiweka siku hii kuwa maalum ya maadhimisho kwakuwa tafiti zinaonesha kupungua kwa matumizi ya kondomu katika mikoa mbalimbali, na hivyo kuongeza hatari ya maambukizi mapya ya VVU na magonjwa ya ngono kwa makundi mbalimbali.