Simba: Mchezo na Vipers utakuwa mgumu sana

0
34

Klabu ya Simba imesema mechi ya marudiano dhidi ya Vipers SC kutoka nchini Uganda itakuwa mechi ngumu kwani timu hiyo bado ina nafasi ya kufanya vizuri katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika.

Ameyasema hayo Afisa Habari wa Simba, Ahmed Ally wakati akizungumza na vyombo vya habari kuhusu mechi hiyo ya marudiano itakayochezwa Uwanja wa Benjamini Mkapa, Machi 07 mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

“Vipers bado wana nafasi ya kufanya vizuri japo kwa tabu lakini bado wana nafasi ya kufanya vizuri. Kila mmoja aliona mchezo wetu wa Entebbe pale Uganda walituzidi, walikuwa bora sana siku ile walicheza vizuri sana, sisi ambacho tulifaidika nacho ni kuwa tulikuwa very objective (na malengo) tulienda kwa ajili ya kutafuta kushinda [..] na malengo yalifanikiwa,” amesema msemaji.

Akielezea kuhusu kwanini mechi hiyo imepangwa kuchezwa katikati ya wiki na si wikendi, amefafanua kuwa ratiba inapangwa na CAF, ambapo inasema katika mechi hizo sita za hatua ya makundi, mechi moja ya kila timu itachezwa katikati ya wiki aidha Jumanne au Jumatano.

Ameongeza kuwa ni aibu nzito kwa Klabu ya Simba kuishia katika hatua ya makundi kwani kwa mara kadhaa timu hiyo imekuwa ikifika na kuishia hatua ya robo fainali, hivyo safari hii haitakuwa tayari kwa namna yoyote ile kuishia katika hatua hiyo.

Kikosi cha Simba tayari kimeingia rasmi kambini leo Machi 03, 2023 kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo, ambapo mgeni rasmi anatarajia kuwa Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘Mwana FA’.

Send this to a friend