
Klabu ya Simba imewataarifu wanachama na wapenzi wa mpira wa miguu kuwa mchezo namba 184 dhidi ya Yanga SC uliopangwa kufanyika Juni 15, 2025 upo kama ulivyopangwa.
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa na klabu hiyo, imewataarifu mashabiki ambao walinunua tiketi ya mechi ya Simba na Yanga iliyoahirishwa Machi 8, 2025 wazitunze kwa ajili ya matumizi ya mchezo wa dabi hiyo Juni 15, 2025.
“Tunawasihi msihadaike na kelele za mitaani, wale ambao walinunua tiketi za mechi ya Machi 8, 2025 wazitunze kwa ajili ya matumizi ya mchezo huo na wale ambao hawajanunua tiketi wajiandae kununua baada ya tangazo la Bodi ya Ligi,” imesema Simba SC.
Aidha, Simba SC imeomba Bodi ya Ligi na TFF watoe hadharani ripoti ya uchunguzi juu ya wote waliohusika kuharibu mechi ya Ligi Kuu, jioni ya Machi 7, 2025 na wachukuliwe hatua.
“Kutotolewa kwa ripoti na kutochukuliwa hatua kwa wanaoendelea kuchochea ghasia ni sawa na kulinda uharamia katika mpira ambao unatia dosari mafanikio yaliyopo katika tasnia ya mpira wa miguu nchini kwa sasa,” imesisitiza.







