Baada ya aliyekuwa kocha wa klabu ya Simba SC kuiaga timu hiyo hivi karibuni, makocha zaidi ya 100 kutoka sehemu mbalimbali duniani wametuma wasifu zao kwa ajili ya kuomba kazi ya kuifundisha timu ya hiyo.
Kikao cha kwanza tayari kimeketi kwa ajili ya kufanya mchujo wa majina hayo na kuangalia wasifu wa kila mmoja na kubaki majina 40 ambao wataingia kwenye hatua ya pili.
Kwa mujibu wa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalez idadi kubwa ya makocha waliotuma wasifu wao ni kutoka barani Ulaya na Amerika ya Kusini.
Ameongeza kuwa mchakato wa kumpata kocha mpya utakamilika ndani ya wiki mbili na atatua nchini kuangalia mechi za mwisho za ligi ili kuona mapungufu na kusimamia usajili.
Aidha ameeleza, wangetamani kupata mzawa wa bara la Afrika lakini mpaka sasa aliyetuma wasifu ni mmoja pekee ambaye kwa bahati mbaya hana vigezo vinavyotakiwa.
“ Tunahitaji kocha anayejua vizuri soka la Afrika, pia tungefurahi kupata kocha ambaye ni mzawa wa bara hili, lakini hadi sasa bado hawajatuma wasifu na aliyetuma ni mmoja na vigezo vyake havitoshi,” amesema Gonzalez.