Simbachawene: Gari la zimamoto kuwa na maji muda wote sio sawa kitaalamu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene amesema kitaalamu gari la kuzimia moto kuwa na maji muda wote sio sahihi kwani itapelekea uharibifu wa chombo hicho.
Akitoa tathmini ya mafanikio ya wizara hiyo kwa miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania, Simbachawene amebainisha kuwa maji ya kuzimia moto yanatakiwa kuwa katika jengo linaloungua, au jengo la jirani au kwenye mtaa ambapo jengo hilo lipo.
“Hivi gari ulibebeshe maji lita 7,000, moto haujawaka miezi mitatu, kuna gari hapo? Limebeba mzigo tu, springs zinaanza kufa. Gari lile ni mtambo, ni mashine ya kwenda kuunganisha na kuzima moto,” amesema waziri huyo akifafanua kuwa mifumo ya maji inatakuwa kuwepo kila mtaa.
Amesema kwa sasa magari hayo huwa na maji ya kuanzia tu, na tegemeo ni kwamba yakiisha, eneo la jirani yatakuwepo, lakini wakati mwingine yanakosekana.
Ametumia jukwaa hilo kukanusha madai kuwa magari ya zimamoto huenda kwenye ajali za moto yakiwa hayana maji.
“Sayansi ya uzimaji moto, maji yatakayozima moto ni yale yatakayokutwa pale. Kwa hiyo hata kama gari litaenda bila maji linategemea kutumia bomba la jirani, lichukue maji likazime moto… Lakini sio kwamba wanaenda bila maji,” ameeleza.
Kumekuwepo malalamiko mara kadhaa kutoka kwa wananchi kuwa magari hayo hufika eneo la tukio kwanza kwa kuchelewa, na wakati mwingine yakiwa na maji kidogo au yasiwepo kabisa.