Jinsi ya kutambua kama WhatsApp yako ina virusi na namna ya kuviondoa
Jumla ya simu milioni 25 zinazotumia mfumo endeshi (OS) wa Android zimeathiriwa na kirusi ambacho huweka ndani ya programu tumishi kama vile WhatsApp na nyinginezo, na kuweka matangazo katika simu hizo, watafuti wa uhalifu wa mitandaoni wameleza.
Kirusi hicho kilichopewa jina Agent Smith kimetumia udhaifu uliokuwepo katika mfumo wa zamani wa Android, na hivyo kufanya kuhuisha mfumo huo (update) kuwa jambo la lazima, kampuni ya ulinzi, Check Point ya Israel imeeleza.
Takribani watu milioni 15 walioathiriwa wapo nchini India, huku 300,000 wakiwa nchini Marekani, na 137,000 nchini Uingereza, na hivyo kufanya pigo hilo kuwa moja ya athari kubwa zaidi kuwahi kuupata mfumo endeshi wa google katika siku za karibuni.
Kirusi hicho kimesambaa kupitia tovuti ya 9apps.com inayomilikwa na Alibaba ya China ambayo watu huweza kupakua programu tumishi kutoka huko.
Kirusi hicho hujificha nyuma ya programu tumishi na hivyo utaweza kuona matangazo unapofungua programu hizo kama vile WhatsApp jambo ambalo sio la kawaida. Ni vigumu kukiona kirusi hicho kwani nembo (logo) yake katika simu haionekani kwa sababu hujificha nyuma ya programu nyingine.
Ili kujihakikishia usalama wa simu yako, endapo unaona vitu visivyo vya kawaida mfano matangazo unapofungua WhatsApp, kuna hatua kadhaa za kufuata.
Kwanza, fungua setting katika simu yako, kisha App and Notifications, kisha App Info. Endapo utaona programu kama Google Updater, Google Installer for U, Google Powers na Google Installer, ziondoe (uninstall).
Pia epuka kupakua (download) programu zisizo rasmi katika tovuti ambazo sio rasmi.