Sita wafariki ajalini Arusha

0
53

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amethibitisha kutokea kwa vifo vya watu sita na wengine wanne kujeruhiwa katika ajali ya gari iliyohusisha gari aina ya Toyota Noah yenye (T 189 DFY) iliyogongana na lori aina ya Scania (T 250 CAA) katika eneo la Alkatani, Monduli mkoani Arusha.

Kamanda Masejo amesema ajali hiyo imetokea Aprili 19, 2022 katika barabara ya Arusha Babati saa nne usiku, na kutaja chanzo cha ajali kuwa ni uzembe wa dereva wa lori ambaye alishindwa kulimudu gari na kuhamia upande mwingine wa barabara kisha kuigonga Toyota Noah.

Ameeleza kuwa bado wanaendelea kufanya uchunguzi kufahamu majina halisi ya abiria waliofariki katika ajali hiyo, pia ameomba wananchi kufika katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Arusha Mount Meru kutambua miili ya marehemu.

Aidha, polisi wanamshikilia dereva wa lori aliyesababisha ajali hiyo na kutoa wito kwa watumiaji wa vyombo vya moto kuwa waangalifu wakati wa matumizi ya vyombo hivyo ili kupunguza ajali ambazo zinagharimu Maisha ya watu.

Send this to a friend