“Simu yangu inazo WhatsApp zenye ushahidi na Katibu Mkuu wetu wa CCM anahafamu yote. Chama kimelazimika kufanya mabadiliko ya viongozi kutokana na mwenendo usioridhisha na hakitasita kuchukua hatua,” amesema Kanali Mstaafu Lubinga.
Lubinga ambaye Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ametoa tahadhari hiyo wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza Kuu la Wazazi ambapo amesema kuwa uchaguzi wa ndani ya chama na jumuiya zake utafanyika mwakani 2022.
Ametumia nafasi hiyo kuwaonya watu walioanza kupanga safu ya viongozi kabla ya muda wa uchaguzi kwamba ni kinyume na maadili ya chama hicho.
“Iko minong’ono miongoni mwenu mmeanza kupiga kampeni, hii ni kinyume cha maadili ya chama chetu na Jumuiya. Kibaya zaidi tunasikia watu wanabeba viongozi na wengine wameshaanza kutoa na kupokea rushwa, ni vema ukaacha wala usithubutu, hakuna kisichofahamika,” amesema.
Licha ya onyo hilo hakuweka wazi taarifa wala jumbe za hao wanaodaiwa kuanza mchakato wa uchaguzi ndani ya chama mapema.