Songwe: Tuta la kuzuia maji lililogharimu TZS milioni 100 lasombwa na maji

0
41

Mkuu wa Mkoa wa wa Songwe, Omary Mgumba amefanya ziara ya ghafla katika Kata ya Kanga wilayani Songwe baada ya kupata taarifa ya tuta lililogharimu shilingi milioni 100 kwa ajili ya kuzuia mafuriko kusombwa na maji.

Aidha tuta hilo ambalo lilikuwa na urefu wa meta 142, lilileta athari ya mafuriko katika mashamba ya wananchi baada ya kusombwa na maji, pamoja na tishio la kukatika kwa mawasiliano ya barabara ya Mbalizi hadi Mkwajuni katika eneo la Kanga.

Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Simon Simalenga amesema baada ya maji kubomoa tuta ambalo lilijengwa kwa ajili ya kuimarisha kingo za mto, maji yalikosa mwelekeo na kuvamia mashamba ya wananchi na kuharibu mazao.

“Nilipotembelea hapa juzi, tulikuta tuta limeliwa kidogo kama meta 30 hivi, lakini jana maji yaliongezeka na kusomba tuta lote na maji,”amesema Simalenga.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe amewaagiza wakala wa barabara kuongeza ukubwa kwa kupandisha juu zaidi tuta la barabara hiyo yenye urefu wa kilometa sita ili maji yasiweze kulifikia katika eneo hilo.

Meneja wa TANROADS Mkoa wa Songwe, Yohana Kasaini alisema utekelezaji wa maagizo hayo utaanza mara moja na kuongeza kuwa tatizo limekuja baada ya mkandarasi aliyekuwa akijenga barabara hiyo mwaka jana kusombwa na maji akiwa bado yuko kazini, na kuongeza kuwa wanatarajia kuomba kiasi cha shilingi bilioni 1 ili kufanikisha agizo la Mkuu wa Mkoa.

 

Send this to a friend