Spika Job Ndugai: Rais Magufuli atake asitike ataongezewa muda Bunge la 12

0
45

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amesema kuwa Rais Dkt Magufuli ataongezewa muda wa kukaa madarakani hata kama yeye mwenyewe hataki.

Ndugai ameyasema hayo bungeni mjini Dodoma wakati akitoa maoni kuhusu hoja ya Mbunge wa Nkasi Kaskazini kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Ally Keissy ambaye amependekeza katiba ibadilishwe ili kuruhusu Rais Magufuli aongezewe muda.

“Mheshimiwa Keissy ngoja tuende uchaguzi mkuu, turudi, na mimi naamini sote tunarudi. Hilo ulishikie uwe nalo moyoni, tutarudi hapa [bungeni] salama, azimio hilo utakuja kulileta wewe Mzee Keissy na litapita kwa kishindo, atake asitake [Rais Magufuli] tutaongeza muda,” amesema spika.

Akitoa hoja yake mbunge huyo amesema kuwa katiba sio msaafu kwamba haifai kubadili, na kwamba inaweza kubadilishwa wakati wowote, na hatokuwa rais wa kwanza kuongezewa muda.

Keissy amesema kuwa kiongozi huyo wa nchi alazimishwe kuendelea kubaki madarakani hata kama hataki, kwani akiondoka yeye nchi itakwenda kubaya. Amesema mara nyingi anapoulizwa nani anafuata baada ya Rais Magufuli, amekuwa akijibu kuwa ataongezewa muda atake asitake.

“Haiwezekani kumuachia nafasi aseme amekataa, amekataa kwa vipi? Alazimishwe tu,” amesema mbunge huyo wa Nkasi Kaskazini.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais anatakiwa kushika madaraka kwa kipindi cha miaka mitano, na anaweza kugombea kwa mihula miwili tu.

Mara kadhaa Rais Magufuli amewewahi kusema kuwa hana mpango wa kuongeza hata dakika tano muda wake wa kuongoza utakapomalizika kwani anaheshimu katiba ya nchi na sheria zote, na pia kazi ya urais ni ngumu.

Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam Juni 13, 2018 muda mfupi baada ya kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM, Humphrey Polepole, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho alisema Rais Magufuli hafurahishwi na mjadala unaoangazia uwezekano wa yeye kubadili kipindi cha urais kutoka miaka mitano hadi saba.

“Jambo hili ndugu mwenyekiti amelieleza kwanza halipo kwenye katiba ambayo yeye aliitumia kuapa na halijawahi kujadiliwa katika kikao chochote cha uongozi. Mwenyekiti amenielekeza niwajulishe wana-CCM walipuuze, halina mustakabali katika maendeleo ya taifa letu,” alisema Polepole.

Mkutano wa 19 wa Bunge la 11 unatarajiwa kufikia ukomo Juni 19 mwaka huu, ambapo Rais Dkt Magufuli atatoa hotuba ya kuvunja bunge, tayari kwa nchi kujiandaa na uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 2020.

Send this to a friend