Spika Tulia awataka viongozi wa Serikali kuzima magari yao ili kubana matumizi ya mafuta

1
14

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson amewasihi viongozi kote nchini, isipokuwa wale ambao itifaki hairuhusu, wazime magari yao wanapokuwa hawayatumii, mfano wakiwa kwenye vikao, ili kupunguza gharama za mafuta.

Dkt. Tulia ameyasema hayo leo Mei 17, 2022 bungeni Dodoma akieleza kwamba gharama za mafuta kwa serikali zimeendelea kuwa kubwa kutokana na viongozi kuacha magari yakiunguruma kwa muda mrefu.

“Tunatamani tuone magari ya kiongozi, yakishamshusha kiongozi, sio tu hapa bungeni, nchi nzima, awe ni mwenyekiti wa halmashauri, awe ni meya, awe ni katibu mkuu, ukiacha viongozi ambao kwa itifaki magari yao inabidi yaendelee kuwaka, magari mengine yakishamshusha kiongozi yazimwe na dereva ashuke,” amesema Dkt. Tulia.

Ametolea mfano watu wanavyozima magari yao wanapokuwa kwenye foleni, na kuhoji kwanini wanaona ni sahihi kuacha gari la serikali likiunguruma hata saa mbili wakati kiongozi hayupo kwenye foleni.

Kauli ya kiongozi wa mhimili huo imekuja wakati changamoto ya mafuta ikiendelea kuikabili dunia, adha ambayo kwa kiasi kikubwa imetokana na janga la UVIKO19, vita vya Urusi na Ukraine na siasa za nchi wazalishaji wakubwa wa mafuta duniani (OPEC).

Send this to a friend