Spika wa Bunge la Uganda awataka Wabunge kuepuka ngono kipindi cha Bunge

0
13

Spika wa Bunge la Uganda, Rebecca Kadaga amewashauri wabunge wa nchini humo na maafisa wa itifaki kulinda hadhi zao na kufuata maadili wakati wote wa Mkutano wa 64 wa Bunge la Jumuiya ya Madola unaotarajiwa kufanyika nchini humo baadae mwezi huu.

Mkutano huo, uliopangwa kufanywa kati ya Septemba 22 na 29 mjini Kampala, unatarajiwa kuhudhuriwa na wajumbe takribani 1,000 ambao unajumuisha maspika na wabunge kutoka mataifa yote 180 ya Jumuiya ya Madola.

Katika hotuba yake kwa wabunge na maafisa wa itifaki kabla ya mkutano huo, Kadaga alisisitiza kuwa nidhamu ni jambo la kwanza, kuheshimu kanuni kuhusu mavazi ya bunge kwa kutovaa nguo fupi na kuwatahadharisha kuhusu kujihusisha na ngono na ujumbe watakaofika.

“Epukeni kufanya ngono hovyo na ujumbe utakaokuja kwenye mkutano. Sitaki kuona Mbunge wangu akipewa ujauzito na Mbunge wa Jamaica ambaye wanaweza wasionane tena.” Pia amewataka viongozi hao kuepuka kuvaa nguo fupi na pia kutokujaza chakula kwenye sahani zao.

Kadaga ameona kuwa weledi unahitajika miongoni mwa maafisa wa itifaki katika kipindi hicho ili kuepuka mazingira yenye kukanganyana kati ya ujumbe na wenyeweji.

”Mtakapo wapeleka wageni kwenye vyumba vyao, simama mlangoni, unaweza kuingiza mizigo ukiwa sambamba na mhudumu wa hoteli. Fanyeni kazi yenu na muondoke,” Kadaga alieleza.

”Matumizi ya pombe yafanyike nyumbani na si kwa wingi, kuepuka harufu ya pombe asubuhi, kuna wakati tulikuwa na upungufu wa magari kisha tukaazima gari kutoka kwa mmoja wa wabunge, ilikuwa na chupa za bia na nyingine zikiwa zimemwagika na kumfikia spika wa Oman,” alibainisha Kadaga.

Send this to a friend