Spika wa Bunge la Marekani, Nancy Pelosi amewasili Taiwan ambapo anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa eneo hilo kabla ya kuondoka katika eneo hilo Agosti 3 mwaka huu.
Pelosi amewasili kwenye eneo hilo licha ya kuwepo kwa katazo na vitisho kutoka China kwamba ziara hiyo ni ukiukwaji wa sera ya China Moja ambayo inaitambua Taiwan kama eneo la China.
Wizara ya Mambo ya Nje wa China imesema kitendo hicho kitakuwa na madhara makubwa katika msingi wa kisiasa wa ushirikiano kati ya China na Marekani, kwani inaingilia milki ya China.
China imeionya Marekani kuacha kuingilia masuala ya ndani na kwamba isitishe mara moja njia inayoiendea kwani ni hatari.
Ofisi ya Rais wa Taiwan imeeleza kwamba inaamini ziara hiyo itaimarisha uhusiano na Marekani na inalenga kuimarisha amani na utulivu katika ukanda huo wa Bahari ya Pacific.