Sportpesa: Yanga imekiuka mkataba kwa kuzindua jezi za mdhamini mpya

0
74

Uongozi wa SportPesa umesema imesikitishwa na uamuzi uliochukuliwa na uongozi wa Klabu ya Yanga wa kukiuka makubaliano yao ya kimkataba kwa kuzindua jezi mpya zenye jina la mfadhili mwingine.

Katika taarifa hiyo iliyotolewa Februari Mosi, 2023 SportPesa imewafahamisha wateja wake na umma kuwa bado ni mdhamini mkuu wa klabu, na ina haki ya kipekee ya kuwa kifuani mwa Yanga SC kwa miaka ya soka 2022 hadi 2025.

“Ombi la Yanga kupata mfadhili mwingine kwa ajili ya hatua inayofuata ya mashindano ya CAF ilikuwa ni kukiuka makubaliano yetu na lilikatisha tamaa sana lilipowasilishwa kwetu. SportPesa inafahamu kikamilifu maagizo na sheria za CAF kuhusu utangazaji/ufadhili uliopo na ilikuwa imetumia kauli mbiu ya ‘Visit Tanzania’ kuchukua nafasi yetu ili kufuata masharti yanayohitajika kutoka kwa CAF,” imesema SportPesa.

Taarifa imeongeza kuwa “kampeni hii mbadala ya ‘Visit Tanzania’ ilifanikiwa kuitangaza nchi nzima kwa misimu miwili iliyopita ya CAF, lakini pendekezo letu lilikataliwa kwa kuwa ilikuwa tayari imeamua kuuza haki hizi bila kujali masharti ya kimkataba yaliyopo na SportPesa.”

Aidha, SportPesa imesema inahifadhi haki yake ya kuomba fidia na msaada kutoka kwa mamlaka husika kwa uharibifu uliosababishwa.

Send this to a friend