Shirikisho la Muziki Tanzania (SMT) limesema kwamba limepokea kwa mikono miwili maoni na ushauri wa wasanii na wadau mbalimbali wa tasnia hiyo kuhusu kukaa kikao, kuchukua uamuzi wa pamoja kuhusu kumpitisha Steve Nyerere au kutafuta Msemaji Mkuu mwingine.
Taarifa ya Katibu Mkuu wa SMT, Farid Kubanda, maarufu Fid Q, imeeleza kwamba kikao hicho kitafanyika Machi 21 mwaka huu na kutoa wito kwa wasanii na wadau wengine kufika ili kujadiliana kwa pamoja na kufikia muafaka.
TAMKO jipya lenye marekebisho..
Nitumie fursa hii kuwashukuru wote mliolipiga SPANA lile jingine, kwa maana limenifunza kitu kuhusu ukurupukaji, uzembe ule hautojirudia..tafadhali pokeeni hili,na kisha mnisaidie kulisambaza.. ninatanguliza shukrani 🙏🏾 pic.twitter.com/wTo8VfF1b1
— #SHUJAA (@FidQ) March 19, 2022
Aidha, SMT imesema isingependa kuwepo mwendelezo wa kashfa kuwa wasanii hawajitambui kwani linaamini kashfa hiyo inaletwa na wasanii kujiweka kando au mbali na mamlaka za kuaamua mustakabali wa maisha yao.
Hatua hii imekuja baada ya kuibuka mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii baada ya shirikisho hilo kumteua Steve Nyerere kuwa msemaji wake.
Wakosoaji wengi walionesha kushangazwa na uteuzi huo na kueleza kwamba wapo wanamuziki wengi ambao wangeweza kushika nafasi hiyo badala ya kuteua mhusika asiyehusika na muziki.