SUA kuwafundisha panya kutambua virusi vya Corona

0
22

Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) wamesema kuna uwezekano mkubwa wa panya wakatumika kwenye kutambua maambukizi ya virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID19.

Hayo yamebainishwa na Mtafiti Mwandamizi na Meneja Mradi wa Utafiti wa Panya wa SUA-APOPO, Dkt. Georgies Mgode kwenye Maonesho ya Ubunifu na mashindano ya Kitaifa ya Sayansi Teknolojia na Ubunifu (MAKISATU 2021) jijini Dodoma.

“Tunaamini panya wanaweza kutambua virusi vya Corona na maambukizi yake kwa ufanisi mkubwa maana tumeshaona mafanikio kwenye utambuzi wa ugonjwa wa kifua kikuu, kwani kila kimelea kina harufu yake na kila ugonjwa unaosababishwa na vimelea tofauti una harufu yake kwahiyo tunaamini Panya wanaweza kufanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa sana,” amebainisha Dkt. Mgode.

Amesema tayari wameshaandika maandiko ya kutafuta fedha kwa ajili ya kuanza kazi ya kufundisha panya hao na zikipatikana wataanza lakini wanaamini watasaidia hasa kutambua wale watu ambao wana vimelea lakini dalili hazijajitokeza maana ukiweza kutambua ugonjwa kabla dalili hazijajitokeza ni rahisi kuzuia maambukizi kwa haraka zaidi.

Amesema kuna wanasayansi wengi huko nchi zilizoendelea baada ya kuona mafanikio makubwa ambayo panya wamefikia walifanya majaribio ya kutumia pua bandia (electronic Nose) kunusa ili kutambua vimelea lakini hawajafanikiwa kama ambavyo SUA wamefanikiwa kwa kumtumia Panya mwenyewe hivyo wataendelea na Panya kutokana na uwezo wake mkubwa katika kutambua.

Mtafiti huyo amesema kwa sasa tusiangalie ni silaha ipi iliyotumika katika kupata matokeao ya ushindi na ugonjwa utakapotokomea ndipo wengine wataamini kuwa mbinu na teknolojia gani inafanya kazi vizuri.

Mradi wa SUA – APOPO unaofanya tafiti za Panya ulio katika kituo cha Udhibiti wa Viumbe Hai Waharibifu ulianza na utafiti wa Panya kwenye kugundua mabomu yaliyotegwa ardhini na ukawa na mafanikio makubwa kwa kuwatumia kwenye nchi mbalimbali duniani hasa za Msumbiji, Angola na Kambodia. Kutambua vimelea vya kifua kikuu,Kutambua utoroshaji wa nyara za Serikali kama pembe za Ndovu na faru pamoja na magamba ya kakakuona,Utoroshaji wa Miti ya mbao ngumu ambayo ipo hatarini kutoweka kwa magendo mipakani.

Send this to a friend