Serikali ya Sudan Kusini imechukua hatua za haraka kwa kufunga shule zote kwa muda usiojulikana kutokana na wimbi la joto ambalo linatishia kufikia hadi digrii 45 Celsius (113 Fahrenheit) ili kulinda afya na usalama wa wanafunzi.
Kwa mujibu wa mamlaka za afya na elimu, wazazi pia wamepewa wito wa kuhakikisha watoto wao wanazuiliwa kutoka nje kwa muda mrefu ili kuzuia madhara yanayoweza kusababishwa na joto hilo la kupindukia.
Aidha, mamlaka hizo zimetoa onyo kali kwa shule zitakazokwenda kinyume na agizo hilo la kufunga shule, kwani shule hizo zitapoteza usajili wao.
Wizara ya afya imeeleza kuwa wiki iliyopita pekee, takribani watoto 15 waliripotiwa kufariki kutokana na magonjwa yanayohusiana na joto, ikiwa ni pamoja na homa ya uti wa mgongo.