
Serikali ya Sudan Kusini imekanusha madai kwamba Rais Salva Kiir alimwelekeza Raila Odinga, kupata idhini ya Rais wa Uganda, Yoweri Museveni kabla ya kukutana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini, Dkt. Riek Machar.
Odinga aliteuliwa kuwa mjumbe maalum wa Sudan Kusini ambapo alikwenda Juba siku ya Ijumaa kwa lengo la kusuluhisha mgogoro unaoendelea nchini humo, ambao umesababisha Dkt. Machar kuwekwa kizuizini kwa agizo la Rais Kiir.
Hata hivyo, katika taarifa iliyotolewa na Katibu wa Vyombo vya Habari wa Rais wa Sudan Kusini, David Amour Majur amekanusha madai hayo na kuyaita upotoshaji wa kanuni na misingi ya diplomasia.
“Pendekezo kwamba Mheshimiwa Jenerali Salva Kiir Mayardit, Rais wa Jamhuri ya Sudan Kusini, alimwomba Mheshimiwa Raila Odinga kukutana na Rais wa Uganda linapotosha kanuni na misingi ya kidiplomasia,” amesema Majur.
Majur amefafanua kuwa ziara ya Odinga nchini Uganda ilipangwa mapema na haikuwa maagizo kutoka kwa serikali ya Sudan Kusini.
Zaidi ya hayo, Sudan Kusini imekanusha madai kwamba Waziri wa Mambo ya Ndani, Angelina Teny ambaye pia ni mke wa Makamu wa Rais, Dkt. Riek Machar yuko kizuizini.