Ikiwa ni siku ya nne kufuatia mapigano makali nchini Sudan, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Khartoum wamenaswa ndani ya majengo ya chuo hicho huku milio ya risasi ikiendelea kusikika karibu na eneo hilo katika mji mkuu wa Sudan.
Mapigano hayo kati ya jeshi la nchi hiyo na kundi la wanamgambo yameenea katika taifa zima lakini eneo hilo la chuo kikuu ni hatari zaidi kwa sababu ya ukaribu wake kambi ya jeshi la ardhi la nchi hiyo.
“Inatisha kwamba nchi yetu itageuka kuwa uwanja wa vita mara moja,” amesema Al-Muzaffar Farouk mwenye umri wa miaka 23, mmoja wa wanafunzi 89 na wafanyikazi wanaojificha ndani ya maktaba ya chuo kikuu.
Sudan: Takriban watu 100 wauawa katika mapigano
Wanafunzi na wafanyakazi wameshindwa kuondoka eneo hilo huku mmoja wao akiuawa kwa kupigwa risasi alipokuwa akijaribu kukimbilia maktaba kutoka jengo la karibu lakini wanafunzi waliufuata mwili wake na kuuingiza ndani licha ya risasi zilizokuwa zikipigwa.
Chuo kikuu kilithibitisha kifo cha Abdulmun’em katika chapisho la Facebook na kuhimiza mashirika ya kibinadamu kusaidia kuwaondoa watu kadhaa waliokwama kwenye chuo hicho cha Khartoum.
Khartoum imekumbwa na ghasia na machafuko katika mzozo wa umwagaji damu wa madaraka kati ya Abdel Fattah al-Burhan, kiongozi wa kijeshi wa Sudan, na Mohamed Hamdan Dagalo, anayejulikana pia kama Hemedti, mkuu wa Kikosi cha wanamgambo cha Rapid Support Forces (RSF) huku takribani watu 200 wakiripotiwa kuuawa katika mashambulizi hayo.