Swahili Times Top Tweeps: Watumiaji Watano Bora wa Twitter Tanzania 2022*

0
41

Mwisho wa mwaka ni wakati ambapo mtu mmoja mmoja, vikundi au familia hupata wasaa wa kuangazia mambo waliyoyafanya kwa mwaka mzima, huku wakiwema mipango ya mwaka unaofuata, wakilenga kufanya makubwa zaidi na kurekebisha makosa yao

Katika makala hii fupi, tunatazama watumiaji watano bora zaidi wa Tanzania ambao wamefanya mambo yaliyokuwa na mchango chanya kwenye jamii. Tafiti zinaonesha kuwa Twitter ndio mtandao muhimu zaidi kwa mijadala ya wazi kwa watumiaji wa mitandao ya kijanii kwenye mambo ta kisiasa, kiuchumi na mengineyo nchini Tanzania.

Mpangilio huu umezingatia vigezo vya nini kilifanywa na tweep husika, ushushuda wa watumiaji wengine wa Twitter na msambao wa maudhui.

1. Flaviana Matata

Kupitia taasisi yake ya Flaviana Matata Foundation mwanamitindo na mfanyabiashara huyo ameendelea kushiriki katika kuboresha sekta ya elimu akishiriki katika ujenzi/ukarabati wa miundombinu ya shule au kutoa vifaa vya kujifunzia kwa wanafunzi.

Mwaka 2022 taasisi hiyo ilikabidhi nyumbani nne za walimu na madarasa katika shule ya Msingi Msinune, Kiwangwa mkoani Pwani. Jitihada hizi zinalandana na azma ya Serikali ya kuendelea kufungua nafasi ya elimu kwa kila mtoto.

2. Carol Ndosi

Mjasiriamali na mtetezi wa haki za wanawake, Kunta amekuwa na mchango mkubwa kwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu masuala mbalimbali ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia ambao unawaathiri wasichana wengi. Moja ya kampeni hizo ni kutoa elimu juu ya madhara ya kutuma picha za utupu, vitendo ambavyo vinaweza kusababisha mwathirika kujiua au kuwa na athari nyinginezo kwenye maisha.

3. Martin Masese

Wakati wote wa kesi ya ugaidi iliyokuwa inamkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na wenzake, Martin alikuwa kiungo muhimu kati ya kilichokuwa kikijiri katika viunga vya mahakama na watumiaji wa Twitter.

Alikuwa akitoa taarifa za kila kilichojiri na kuwezesha watu wengi zaidi kufuatilia kesi hiyo iliyowavuta watu wengi kutoka wanachama wa chama hicho, wanaharakati, mabalozi na taasisi za kimataifa zilizokuwa zikitaka kujua kinachoendelea. Alikuwa ni chanzo cha kuaminika.

4. Michael Baruti

Mara nyingi wanaume si watu wanaozungumzia sana yale wanayopitia katika maisha. Kupitia Men Men The Podcast, Baruti amekuwa akijadili na watu mbalimbali masuala ya kisaikolojia yanayowakabilia wanaume, majadiliano ambayo yanawasaidia wanaume kukabiliana na changamoto za maisha kwanza kwa kupata nafasi ya kuyazungumza, lakini pia wanaposikia namna mtu mwingine alivyokabiliana na changamoto ambayo nao wanaipitia.

5. Tito Magoti

Alipoteza haki ya kupiga kura akiwa mahabusu mwaka 2020, alipotoka akafungua kesi kupinga kifungu cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kinachopingana na Katiba ambayo inatoa haki ya kupiga kura kwa Watanzania wote wenye miaka 18 na zaidi.

Alishinda kesi hiyo baada ya mahakama kutamka kuwa kifungu hicho ni batili na hivyo kuwapa wafungwa wote wenye sifa haki ya kupiga kura katika chaguzi zijazo.

Je! Wewe kwa mwaka 2022 umefanya nini ambacho kimekuwa na matokeo chanya kwenye jamii inayokuzunguka? Tutajie pia yoyote katika mtandao wa Twitter ambaye unampa kongole kwa kufanya jambo lenye tija kubwa kwa jamii kwa 2022.

Heri ya Mwaka Mpya 2023.

Send this to a friend