Taarifa kuhusu kufungwa kwa Daraja la Wami

0
54

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) inakusudia kufunga kwa saa mbili Daraja la Wami lililopo katika Barabara ya Chalinze-Segera kuanzia Juni 25 hadi Juni 27 mwaka huu.

Taarifa iliyotolewa kwa umma na Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Patrick Mfugale inaeleza kuwa daraja hilo litafungwa kwa siku tatu mfululizo kuanzia saa 8:00 usiku hadi saa 10:00 alfajiri.

Mfugale ameeleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa ili kuruhusu ukaguzi mkubwa na matengenezo, na kwamba kwa muda tajwa daraja halitopitika.

TANROADS imeomba radhi kwa usumbufu utakaojitokeza.

Katika eneo hilo ajali zimekuwa zikitokea mara kwa mara na hivi karibuni ilitokea ajali ambayo ilihusisha magari makubwa matatu, magari madogo mawili pamoja na pikipiki.

Hata hivyo, serikali inaendelea na ujenzi wa daraja jipya ambalo tayari mradi huo umekamilika kwa asilimia 49. Kukamilika kwa daraja hilo ambalo ni kiungo muhimu cha kiuchumi katika barabara hiyo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza ajali zinazogharimu maisha ya watu na mali zao katika eneo hilo.

Send this to a friend