Taarifa muhimu kwa waombaji wa mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi Tanzania

0
40

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetoa muda wa siku 5 kuanzia Oktoba Mosi hadi 5 mwaka huu ili kuwawezesha wanafunzi waliomaliza mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) hivi karibuni kuomba mkopo kwa njia ya mtandao na kukamilisha maombi yao.

Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru amesema uamuzi huo unatokana na maombi ya wanafunzi, wazazi na walezi ambao hawakuweza kuomba au kukamilisha maombi yao kutokana na sababu ya kujiunga na mafunzo hayo.

Katika muda huo wa siku tano, mfumo pia utakuwa wazi ili kuwawezesha waombaji ambao maombi yao yana upungufu kurekebisha kwa kuweka nyaraka sahihi ili kuiwezesha HESLB kuendelea na hatua nyingine.

“Kwa wanaorekebisha taarifa, wanapaswa kuingia katika akaunti zao walizofungua kuombea mkopo na watapata ujumbe kuhusu maeneo ya kurekebisha. Tunawasihi watumie muda huu wa siku tano kurekebisha na kukamilisha maombi yao,” amesema Badru.

Katika mwaka wa masomo 2020/2021, Serikali imetenga TZS bilioni 464 zitakazowanufaisha jumla ya wanafunzi 145,000. Kati yao, wanafunzi 54,000 watakuwa wa mwaka wa kwanza na wengine 91,000 ni wanafunzi wanufaika wanaoendelea na masomo.

Mwaka 2019/2020 jumla ya TZS 450 bilioni zilitengwa na zimewanufaisha jumla ya wanafunzi 132,119.

Send this to a friend