Taarifa muhimu ya bodi ya mikopo kwa wanafunzi wa vyuo

0
42

Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imeanza kufanya malipo yenye jumla ya thamani ya TZS 63.7 bilioni ikiwa ni fedha za chakula na malazi kwa ajili ya robo ya tatu ya mwaka wa masomo 2019/2020 na fedha hizo zitawafikia wanufaika wote kupitia vyuo vyao ifikapo Alhamisi, Mei 28, 2020.

Bodi hiyo imesema hatua ya kuanza kufanya malipo inafuatia maelekezo ya kufunguliwa kwa taasisi za elimu ya juu ifikapo Juni 1, 2020 ambayo yametolewa Rais, Dkt. Magufuli jijini Dodoma.

Wakati huohuo, HESLB inakamilisha malipo yenye thamani ya TZS 59.1 bilioni ya ada za wanafunzi wanufaika ambayo yatalipwa kwa taasisi zaidi ya 70 za elimu ya juu zilizopo nchini.

Katika mwaka wa masomo 2019/2020, serikali inatoa mikopo ya elimu ya juu yenye jumla ya thamani ya TZS 450 bilioni kwa wanufaika 132,119. Fedha hizi zinagharamia vipengele sita ambavyo ni chakula na malazi, ada, vitabu na viandikwa, utafiti, mafunzo kwa vitendo, na mahitaji maalum kwa baadhi ya vitivo.

Serikali ilifunga shule na vyuo Machi 16, 2020 kama sehemu ya jitihada za kupambana na maambukizo ya virusi vya corona na ugonjwa wa COVID-19.

Send this to a friend