Taarifa ya Polisi kuhusu kukamatwa kwa Mbowe, Mdee na Zitto watakiwa kujisalimisha
Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema linaendelea na oparesheni kali ya kukamata watu wanaofanya mipango ya kuhamasisha maandamano bila kufuata sheria na kusababisha taharuki kwa wananchi sambamba na mipango ya kuharibu mali, miundombinu na kudhuru watu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema kutokana na oparesheni waliokwisha kuifanya hadi sasa wanawashikilia watu 14 wanaohusishwa na kuratibu maandamano.
Wanaoshikiliwa ni pamoja na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa CHADEMA, Bonface Jacob, aliyewahi kuwa Meya wa Ubungo na mwanachama wa CHADEMA, Denis Vesta, Godfrey Seleman, Elisha Mbandamka na Shehebu Kiarus.
Wengine ni Yohana Marco, Salehe Omary, Mohamed Omary na Godbless Lema, aliyekuwa mgombea ubunge Jimbo la Arusha Mjini.
Aidha, jeshi hilo limetoa dhamana kwa Tundu Lissu na watuhumiwa wengine watatu baada ya kuwahoji na jalada limepelekwa kwa mwanasheria mkuu wa serikali kwa hatua zaidi za kisheria.
Watuhumiwa wengine wanaotafutwa ni pamoja na Halima Mdee ambaye alikuwa mgombea Ubunge jimbo la Kawe kupitia chama cha CHADEMA pamoja na Zitto Kabwe ambaye ni Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo, na aliyekuwa mgombea Ubunge Jimbo la Kigoma Mjini.
Kamanda Mambosasa amesema Jiji la Dar es Salaam liko shwari na amewataka wanasiasa waache tabia ya kwenda kufanya fujo maeneo ambayo sio majimbo yao na hatimaye wafuate sheria ili kupeleka malalamiko yao Tume ya Taifa ya Uchaguzi.